Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wataalamu hao wametoa ombi hilo kwenye mkutano wa WTO unaoendelea mjini Geneva Uswisi kujadili masuala ya haki miliki.
Wamehimiza ushirikiano mkubwa katika fursa za kupata chanjo za COVID-19 kote duniani, huku wakiweka bayana hali halisi ya mgawanyiko, pengo la usawa, na maslahi ya kitaifa na ya kikanda katika chanjo hizo.
Wameongeza kuwa mabilioni ya watu hususan katika mataifa yanayoendelea wanaweza kukosa chanjo ya COVID-19 hadi mwaka 2024 na hii si haki. Wameziomba nchi zilizoendelea kukomesha utaifa na ubinafsi katika chanjo ambavyo vimekuwa vikichochea mgawanyiko na kuathiri juhudi za kujikwamua na janga hili kote duniani.
Kundi hilo la wataalamu wa haki za binadamu limesema mkakati wa kimataifa wa chanjo COVAX, ni hatua muhimu kuelekea utaratibu maalumu wa kusambaza chanjo duniani kote.
Shirika la Afya duniani WHO linakadiria kwamba asilimia 95 ya chanjo za COVID-19 ambazo zimezalishwa hadi sasa zimeenda katika nchi 10 tajiri duniani.
Jopo hilo la wataalamu linasema: “Hili ni dhihirisho la kushindwa kutoa ushirikiano ambao unaathiri haki ya maendeleo kwa kila mtu na kwa watu wote.”
Wataalamu hao pia wamesema janga la COVID-19 ni changamoto ya kimataifa ambayo inaweza kutatuliwa tu kupitia juhudi na hatua za pamoja.
342/